Rais wa Kenya William Ruto alitembelea Ijumaa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote jijini Lagos, Nigeria, kabla ya hafla ya uwekaji jiwe la msingi wa mradi mpya wa kiwanda cha kusafisha mafuta mjini Lamu, Kenya.
Ruto alifanya ziara hiyo katika kiwanda hicho chenye thamani ya dola bilioni 20 za Marekani kwa mwaliko wa Rais na Mtendaji Mkuu wa Dangote Industries Limited, Aliko Dangote.
Alikielezea kiwanda hicho cha Nigeria kama kielelezo cha kile ambacho serikali za Afrika, wawekezaji na taasisi za fedha zinaweza kufanikisha zinaposhirikiana.
Kwa mujibu wa Ruto, kiwanda cha Kenya, ambacho ujenzi wake umepangwa kuanza wiki ijayo, kitakuwa kikubwa kuliko mradi wa Nigeria.
Rais huyo alisema Kiwanda cha Kusafisha Mafuta cha Dangote Afrika Mashariki (Dangote East African Refinery) kinachopangwa kujengwa Lamu kitaleta mageuzi katika sekta ya mafuta ya Kenya na kuimarisha upatikanaji na usalama wa mafuta katika ukanda mzima.
Ruto alieleza kuwa mradi huo pia utachochea ukuaji wa viwanda na kuzalisha takriban nafasi 60,000 za ajira utakapokamilika.
Aliongeza kuwa kiwanda hicho kitafungua fursa za kuendeleza viwanda vinavyohusiana, vikiwemo vya kutengeneza mbolea, kemikali na vifungashio.
Akielezea ukubwa wa kiwanda cha Nigeria, Ruto alisema kina uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 ya mafuta ghafi kwa siku na huzalisha zaidi ya lita milioni 100 za petroli, dizeli na mafuta ya ndege kila siku.
Pia alibainisha kuwa Kundi la Dangote (Dangote Group) lilijenga kilomita 120 za nyaya za baharini (sea cables) ili kurahisisha usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka kwenye meli hadi kiwandani.
Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Ruto aliandika: “Mafanikio haya makubwa ni ushahidi wa kile ambacho serikali za Afrika, wawekezaji na taasisi za fedha wanaweza kufanya kwa pamoja.”
Comments
0