Mohamed Salah hatasafiri na kikosi cha Misri kwenda Sudan Kusini kwa mchezo wao wa pili wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), kwa sababu mechi hiyo itachezwa kwenye uwanja wa nyasi bandia. Shirikisho la Soka la Misri (EFA) lilitangaza uamuzi huo Jumamosi.
Mchezo kati ya Sudan Kusini na Misri utafanyika katika Uwanja wa Juba, ambao sehemu yake ya kuchezea imetengenezwa kwa nyasi bandia (artificial turf).
Kupitia mitandao ya kijamii, EFA ilisema: “Benchi la ufundi la timu ya taifa ya Misri, likiongozwa na Hossam Hassan, limeamua kumpumzisha Mohamed Salah katika mechi dhidi ya Sudan Kusini iliyopangwa kufanyika Septemba 29 kwa sababu ya uwanja wa kuchezea.”
“Ilikubaliwa kati ya benchi la ufundi la timu ya taifa na Mohamed Salah kabla ya mechi dhidi ya Angola kwamba hatacheza dhidi ya Sudan Kusini, na benchi la ufundi lilipendelea njia hii ili kumlinda mchezaji,” EFA iliongeza.
Katika mchezo wao wa kwanza wa kufuzu uliochezwa Ijumaa, Misri ililazimishwa sare ya bila kufungana na Angola kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
Salah, ambaye hivi karibuni alijiunga na Trabzonspor ya Uturuki akitokea Liverpool, alianza katika mchezo dhidi ya Angola, lakini hakuumaliza baada ya kocha Hossam Hassan kumtoa katikati ya kipindi cha pili.
Comments
0